Haki za uzazi katika sheria mpya ya kazi Tanzania hizi hapa
Haki za uzazi katika sheria ya kazi Tanzania hizi hapa
February 17, 2017
tv malezi
Malezi katika zama za utandawazi na runinga/TV
March 1, 2017
Show all

Ijue nafasi ya wazazi na watoto katika kurithi mali za wapendwa wao..

Mirathi muislamu

Makala haya ni muendelezo wa makala yetu ya Jumapili iliyopita ambapo tuliangalia sheria zinazohusu urithi na wosia, yaani mirathi. Tulieleza kuwa sheria za makundi matatu hutumika. Mosi ni la Sheria ya Serikali, alafu lile la Sheria ya Mila na tatu ni Sheria ya Dini ya Kiislamu. Leo tutaangalia taratibu za mirathi kwa kutumia sheria ya Dini ya Kiislamu kwani zile za serikali na mila tayari tuliziona juma lililopita.

 
Sheria ya Kiislamu ya Mirathi ni kama ilivyoainishwa katika vifungu mabalimbali vya Kuruani Tukufu na kufafanuliwa katika Makala mbalimbali za wanazuoni wa Kiislamu. Hapa Tanzania Bara, Sheria ya Kiislamu ya mirathi imeanishwa katika Tamko la Sheria za Kiislamu la mwaka 1967. Tamko hili pamoja na kwamba halijawahi kutumika rasmi, ni mwongozo mzuri wa Sheria ya Kiislamu. Kama mirathi yeyote ile, mgawanyo wa mali ya marehemu kwa mujibu wa Sheria ya Kiislamu, huzingatia mambo muhimu matatu yafuatayo.

 
Kwamba mwenye mali awe alishakufa (maut al–muwarith), pili pawepo na warithi halali wa marehemu (hayat alwarith) yaani watoto wa marehemu na ndugu wengine wa marehemu. Warithi hawa ni lazima wawepo na wawe ni warithi hakika wanaotambulika kisheria wakati wa mauti ya marehemu. Mwisho kwamba marehemu ameacha mali (al- tarikah I al–mauruth), yaani urithi utokane na mali halisi na halali za marehemu na sio nje ya hizo.

 
Kabla ya mirathi lazima matatizo yafuatayo yawe yametatuliwa kwanza. Lazima madeni yanayokabili mali za marehemu yapewe suluhu. Yaani wote wanaomdai marehemu kihalali hupewa kipaumbele kabla ya kugawa urithi. Gharama za mazishi ziwe tayari zimelipwa kabla ya kugawa mirathi. Wosia lazima ufuatwe kwa kuzingatia warithi halali.

 
Kulingana na mafundisho ya dini ya Kiislamu, wanazuoni wote kwa ujumla wanaafiki makundi yafuatayo kuwa ndio warithi halali kwa mujibu wa dini ya Kiislamu; As’hab Al – Furud ni kundi la watu wanaopata urithi wao kufuatana na muainisho wa bayana uliotolewa ndani ya Kuruani Tukufu. Hawa kwa kawaida wapo kumi na mbili. Kati yao wawili hupatikana kwa njia ya mahusiano ya kinyumba yaani mke na mume, wengine hutokana na undugu wa damu na uhusiano wa ukaribu kindugu, yaani jamaa. Wanajumuisha mume, mke, mtoto wa kiume, mtoto wa kike, mama, dada, kaka, mpwa, dada wa kambo, kaka wa kambo na babu mzaa baba.

 
Asabah ni wale wenye kupata urithi kutokana na albaki ya mali yote baada ya wale warithi waliobainishwa kwenye Kuruani kupata sehemu yao. Kundi lingine linajulikana kama Hazina ya Umma. Wanazuoni wanaoongozwa na Iman Hanafi na Hanbal, wanapinga mali za marehemu kupelekwa katika hazina kusaidia jamii. Lakini wale wenye mtazamo wa mawazo kama ya Malik na Shafii wanaafiki mali ya marehemu kuchukuliwa na kurithishwa kwenye hazina ya jamii. Mali za namna hii huwa ni mali ya jamii nzima na huwa chini ya msimamizi wake mkuu aliyechaguliwa na jamii yenyewe. Mfano katika serikali ya mapinduzi Zanzibar, mali zitolewazo kama Baitul Mal (hazina ya umma), zimewekwa chini ya uangalizi wa Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana. Kundi la mwisho ni Dhawl –Arham, hili ni la wale ndugu wasiotokana na damu ya marehemu moja kwa moja.

 
Tumalizie kwa kuangalia jinsi mgawanyo wa urithi unavyokuwa. Iwapo marehemu ameacha watoto, wajane/mjane hurithi 1/8 lakini kama hapana watoto wajane/mjane hurithi ¼ ya mali. Wazazi hupewa 1/6 ya salio baada ya kuondoa fungu la mjane/wajane. Mali inayobaki baada ya kutoa wajane/mjane na wazazi/mzazi, hugawanywa katika mafungu matatu. Watoto wa kiume hupata mafungu mawili na watoto wa kike hupata fungu moja. Mgane hupewa ¼ ya mali ya marehemu mke wake kama kuna watoto au ½ kama hakuna watoto. Watoto waliozaliwa nje ya ndoa hawana haki ya kurithi kwa baba yao.

 
Izingatiwe kwamba mgawanyo wa mali kwa mujibu wa dini ya Kiislamu, hufuata matabaka kama yalivyobainishwa hapo juu. Kulingana na Sheria ya Kabidhi Wasii Mkuu, endapo mtu atakufa bila kuwa na mrithi, au kwamba mali yake inaweza kupotea, basi hiyo mali itawekwa chini ya Kabithi Wasii Mkuu, na endapo utapita muda wa miaka kumi na mbili bila mtu yeyote kudai kitu chochote kuhusu mirathi hiyo, basi Kabidhi Wasii Mkuu ataihamishia mali hiyo Serikalini.

 
Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org

Facebook Comments