Katika safari ya malezi, wazazi wengi wanakumbana na changamoto ya hatua za ukuaji wa watoto wao. Wengi wazazi hutegemea mtoto wa umri fulani awe na uwezo, mtazamo na uwajibikaji binafsi unaoendana na umri wake. Wakati huo watoto huweza kuwa na fikra, uwezo na matendo tofauti na umri wao.
Katika jitihada za mzazi kuweza kumsaidia mtoto atambue hatua zake za ukuaji, huwa wanawalinganisha na wenzao ndani au nje ya familia. Utaskia mzazi akisema, mwenzako fulani anaweza kufua nguo zake mwenyewe, wewe huwezi kabisa au mwenzako mbona anafaulu hesabu na wewe unafeli wakati mnafundishwa na mwalimu mmoja nk. Hapa ndipo mtazamo wa ukuaji kwa watoto na wazazi hutofautiana.
Kama wazazi, sote tunataka watoto wetu wawe na uwezo wa kukabili changamoto za maisha kwa ufasaha. Jinsi tunavyozungumza na watoto wetu wanaposhindwa au wanapofanikiwa, kunaweza kujenga mitazamo yao juu ya hatua ya ukuaji waliyopo na juu ya maisha kwa ujumla.
Tunaweza kuwajengea mitazamo chanya ya ukuaji ("growth mindset") au mitazamo ambayo ni mgando ("fixed mindset"). Kulingana na utafiti wa mtaalamu wa saikolojia, Dr. Carol Dweck, makala hii itaangazia jinsi wazazi tunavyoweza kuwasaidia watoto wetu kujenga fikra chanya juu ya ukuaji na kuonesha jinsi gani mtazamo huo ni muhimu kwa mafanikio ya muda mrefu.
Kwanza, tufahamu maana ya mtoto kuwa na fikra juu ya ukuaji wake.
Hii ni namna ambavyo mtoto anajichukulia au anavyojitazama katika fikra zake juu ya uwezo alionao kulingana na umri wake. Kuna wanaotambua kuwa kwa umri walionao wanapaswa kuwajibika na kujikumbusha majukumu yao wenyewe na kuyatekeleza kwa ufasaha wakati wengine wakiwa kinyume chao. Katika utafiti wake wa kipekee, Dr. Dweck aligundua kuwa watu wenye mtazamo unaobadilika ("growth mindset") wanaamini uwezo wao unaweza kukua kulingana na juhudi wanazoweka na kwa kujifunza kutokana na makosa yao.
Kwa upande mwingine, watu wenye mtazamo usiobadilika yaani matazamo/fikra magando ("fixed mindset") wanaamini kuwa uwezo wao una ukomo na hauwezi kubadilika. Wanakwepa changamoto kwa hofu ya kushindwa, wakihisi kwamba hawawezi kufanikiwa hata wajaribu vipi.
Utafiti wa Dweck, hasa uliohusu watoto walio na umri wa kwenda shule, ulionesha kuwa watoto wenye mtazamo chanya walikuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kutatua changamoto, hata pale walipopitia wakati mgumu. Mtazamo huu unawasaidia watoto kujifunza uvumilivu na subira, si tu katika masomo, bali pia katika kukabiliana na cahangamoto katika maisha yao ya kila siku.
Tunawezaje kuwasaidia watoto kujenga mtazamo/kuwa na fikra chanya juu ya ukuaji?
Kwa mujibu wa tafiti, zifuatazo ni njia ambazo sisi wazazi tunaweza kuhamasisha watoto wetu kujijengea mtazamo huu wa maisha.
Kwanza tujitahidi kusifu juhudi za mtoto katika jambo flani zaidi ya matokeo yake au kiwango cha akili alichonacho, yaani intelligence kwa lugha ya kimombo. Utafiti unaonesha kwamba kumpongeza mtoto kwa juhudi zake, badala ya kumpongeza kwa akili, talanta zake au matokeo ya alichokifanya, kunaweza kumsaidia kujenga mtazamo chanya. Kwa mfano, badala ya kusema "Una akili sana kwenye hisabati," ni bora kusema, "Umefanya kazi kwa bidii sana kwenye hili somo!" Hii inasisitiza thamani ya juhudi na kujituma, ambayo ndiyo kiini cha mtazamo chanya wa ukuaji na uwajibikaji. Pia hii itampa fikra kwamba ana wajibu wa kufanya ili kuweza kufanikiwa katika jambo husika.
Pili, tuhamasishe ari ya kujifunza vitu vipya. Watoto wenye mtazamo wa ukuaji wanapenda kujifunza na wanachukulia kujifunza kama fursa ya kuendelea, badala ya kazi ngumu. Wazazi tunaweza kukuza ari na upendo huu kwa kuwahamasisha watoto kuuliza maswali, kuchunguza vitu vipya, na kuona kila changamoto kama nafasi ya kujifunza. Tuwakumbushe kuwa kujifunza ni safari ya maisha.
Tuwafundishe watoto kwamba kukosea ni sehemu ya ukuaji. Watoto wanahitaji kuelewa kwamba kushindwa au kukosea si jambo la kuogopa, bali ni sehemu ya kujifunza. Utafiti unaonesha kwamba watoto wanaoona makosa kama fursa za kujifunza, wana uwezo mkubwa wa kuvumilia changamoto za Maisha na kukuza jitihada za kujaribu maradufu hadi wafanikiwe. Badala ya kuwauliza "Kwa nini umekosea?", tunaweza kuwauliza "Umejifunza nini kutokana na hili?" au "Utajaribu nini wakati mwingine?"
Tuwe mfano wa kuigwa kwa kuwa na mtazamo chanya sisi wenyewe. Watoto hujifunza zaidi kutoka kwa tabia na mitazamo ya wazazi wao. Tunapofanya kazi kwa bidii, tunapokubali makosa yetu na kujifunza kutokana nayo, tunawapa watoto mfano mzuri wa kufuata. Tukionesha jinsi tunavyothamini juhudi na kujifunza, watoto wetu watajifunza kufanya hivyo pia.
Tuwapatie Maukumu kulingana na umri wao Pamoja na kuwafuatilia kuhakikisha wanatekeleza. Wazazi tunapaswa kuwapangia watoto majukumu kulingana na umri wao na si kuwafanyia kila kitu, hii itawakuza kifikra kwamba majukumu ni sehemu ya Maisha ya kila mtu lakini pia watapata hisia kwamba wanapiga hatua katika ukuaji wao na watahamasika katika kujitazama tofauti na kwa mtazamo chanya zaidi juu ya hatua za ukuaji na majukumu wanayopaswa kuyatimiza.
Je, sayansi inasemaje kuhusu mtazamo chanya wa ukuaji?
Ufanisi wa mtazamo huu umehakikishwa kupitia sayansi ya neva. Tafiti zimeonesha kwamba ubongo wa binadamu, hasa kwa watoto, unakua na kubadilika mara kwa mara. Kila mara mtoto anapokabiliana na changamoto na kujifunza kitu kipya, ubongo wake unaunda uhusiano mpya wa neva, jambo ambalo linakuza uwezo wake wa kujifunza na kutatua matatizo na kjitazama kwa mtu mwenye wajibu wa kutekeleza.
Dhana hii ya sayansi ya ukuaji wa neva inasisitiza kwamba uwezo wa binadamu unaweza kukua kupitia juhudi na mazoezi. Kwa mfano, utafiti uliochapishwa katika Nature Neuroscience ulionesha kwamba wanafunzi waliokuwa wakifundishwa kuhusu ukuaji wa neva na mtazamo chanya wa ukuaji walifanya vizuri zaidi shuleni, hasa katika masomo kama hesabu, ambayo yanahitaji mazoezi ya mara kwa mara.
Kujenga mtazamo chanya wa ukuaji kwa watoto ni mchakato wa muda mrefu, lakini ni muhimu kuanza mapema watoto wakiwa wadogo, kama ule msemo usemao samaki mkunje angali mbichi. Kama wazazi, tuna jukumu kubwa la kuwasaidia watoto wetu kujenga ujasiri wa kukabiliana na changamoto za maisha, kujifunza kutokana na makosa yao, na kuamini kuwa uwezo wao unaweza kukua kila wanapojituma na kujifunza, namna hii watakuwa na fikra chanya juu ya ukuaji wao.
Kwa maoni na ushauri, tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozwi malipo kutoka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook, Twitter na Instagram @SemaTanzania.