top of page
C-Sema Team

Je, umejipangaje kusafiri na watoto wakati wa likizo za sikukuu?

Tunaendelea na makala zetu zenye maudhui ya malezi wakati wa likizo. Tarehe zile za kusafiri zimefika kwenda kusalimia babu na bibi na ndugu wengine katika maeneo mbali mbali hasa katika maeneo ambayo si makazi yetu ya kila siku, hivyo leo tutazungumzia mbinu kadhaa zitakazotusaidia kusafiri na watoto kwa amani na furaha kulingana na makundi ya umri wa watoto.

Watoto wachanga (miaka 0-2)

Kwa watoto wachanga, maandalizi ni muhimu sana ili kuhakikisha wanakuwa na utulivu safarini. Kubeba nepi/pampasi za kutosha, kanga, nguo za kubadilisha, na blanketi laini ni muhimu. Pia, tukumbuke kubeba vitu vya kuchezea au vitabu vya picha ili kumliwaza mtoto hapa na pale hasa anapokuwa katika mazingira mapya. Watoto wa umri huu mara nyingi hulala muda mrefu safarini, hivyo tuandae mazingira yatakayowafanya wajihisi salama, hasa ikiwa tunasafiri kwa gari au ndege.


Lishe ni jambo la kipaumbele kwa watoto wachanga. Kama mtoto anakunywa maziwa ya chupa, tuhakikishe tunabeba chupa safi, maziwa ya unga, na maji ya moto. Safari za ndege zinapokuwa na mabadiliko ya shinikizo la hewa na hata magari kukumbana na changamoto za dharura za barabarani, kuwa na akiba ya chakula cha kutosha kwa ajili ya mtoto ni muhimu sana na itapunguza usumbufu. Pia kama mtoto bado ananyonya ziwa la mama, ni vyema mama uzingatie lishe yako kwa kubeba chakula na maji ya kutosha au kuwa na akiba ya pesa ya kuhakikisha utapata chakula wakati wa dharura ili kumuwezesha mtoto kunyonya vya kutosha. Usalama ni muhimu pia; tujitahidi kutumia kiti maalum cha gari kwa watoto wachanga, au kibebeo cha watoto kama kanga au kitenge ili kuhakikisha wanafarijika na wanalindwa wakati wote bila kusahau kufunga mikanda ya viti vyetu ili tuwe tayari kuhakikisha usalama wetu pamoja na watoto wetu.


Watoto wa umri wa chekechea (miaka 3-5)

Watoto wa umri huu wanahitaji maandalizi ya kisaikolojia kabla ya safari. Tuwaeleze kwa maneno rahisi kuhusu safari, kwamba wanaenda wapi na kwanini. Ushawishi wa mawazo yao katika kupanga ratiba ya safari huwasaidia kujihisi kuwa sehemu ya safari, hii inaweza kuhusisha kuwaomba watoe maoni kuhusu vitu wanavyotaka kufanya au kuona.

Ili wasisumbuke sana wakati wa safari, tuchukue vitabu vya kuchora, rangi, au midoli wanayoipenda. Hii itawashughulisha na kuwazuia kuchoka mapema. Watoto wa umri huu hula mara kwa mara, hivyo ni muhimu kuwa tayari kwa mahitaji yao ya chakula.  Hivyo, vitafunwa rahisi kama biskuti, matunda yaliyokatwa, na maji ya kunywa vinashauriwa kubebwa. Wakati wa safari, tuhakikishe wanakaa salama kwa kufunga mikanda ya usalama kwenye viti wanavyokalia na kuzingatia harakati zao kwa karibu kuepusha usumbufu kwa abiria wenzetu na kama tupo kwenye usafiri binafsi ili kuepusha madhara yanayoweza kutokea.


Watoto wa umri wa shule (miaka 6-12)

Watoto wa umri wa shule wanaelewa zaidi mambo yanayowazunguka, hivyo kushirikishwa katika maandalizi ya safari ni njia bora ya kuwajumuisha. Tunaweza kuwauliza maswali mbali mbali kuhusu shughuli watakazopenda kufanya au sehemu zipi wangependa kutembelea.

Hawa wanaweza kupewa vitabu vya kusoma, vifaa vya michezo wanayoipendelea lakini muhimu pia kuwahimiza kuangalia mazingira wakati wa safari ili kujifunza zaidi. Watoto wa umri huu pia wanaweza kusaidia katika kubeba mizigo midogo au kuandaa vitu vidogo kwa ajili ya safari hasa vinayowahusu kama nguo zao nk.. Usafi na afya ni muhimu sana, hivyo tuhakikishe wanatumia vitakasa mikono na kufuata kanuni za usafi, hasa mkiwa maeneo yasiyo na maji safi,pia, tuepuke kula vyakula vya njiani.


Vijana wadogo (miaka 13-17)

Kwa vijana, safari ni fursa nzuri ya kuwapatia uhuru wa kuchagua na kuwashirikisha katika maamuzi. Tuwaruhusu vijana wetu wadogo kutusaidia kupanga ratiba ya safari. Hii inaweza kuwa kuchagua maeneo ya kutembelea au shughuli zinazowavutia, kama kutembelea maeneo ya kihistoria au sehemu za burudani.

Kwa kuwa vijana wanapenda kutumia vifaa vya kidijitali, hakikisha betri za simu au tablets zimejaa kwa ajili ya kujiliwaza na kuchukua matukio ya kumbukumbu ya safari huku ukihakikisha hawatumii muda mwingi kwenye vifaa hivyo bali tuwapatie muda wa kuzungumza nao kuweza kuwafahamu zaidi mawazo yao juu ya mambo mbalimbali ya maisha na dunia kwa ujumla, malengo, na changamoto wanazokutana nazo. Hii itatusaidia kuongeza ukaribu nao na kufurahia safari Zaidi, kitu ambacho kitaweka kumbukumbu nzuri ya mahusiano yao na wazazi/walezi wao.


Safari nyingi nzuri hupangwa mapema, hivyo tujipange kwa wakati, kwa kukata ticketi na kuthibitisha sehemu za malazi mapema. Pia tujitahidi kufahamu sheria za usafiri zinazohusiana na watoto, kama vile kanuni za LATRA zinazoruhusu watoto wenye umri chini ya shule ya msingi kusafiri bila malipo katika mabasi, pia tufahamu hospitali au vituo vya afya vilivyo karibu na maeneo tutakayofikia kwa ajili ya usalama wetu na wa watoto wetu.

Tunawatakia safari njema zenye furaha tele.


Kwa maoni na ushauri kuhusu masuala ya watoto, piga simu namba 116 bila malipo. Pia, unaweza kututembelea kupitia mitandao yetu ya kijamii: Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania, au tovuti: www.sematanzania.org.

 

 

0 views
bottom of page