top of page
C-Sema Team

Je, unajua kwamba ratiba ya kulala kwa mtoto huimarisha umakini, uwezo wa kukumbuka, na uwezo wake wa kufanya maamuzi.


Kulala, kwa maana ya kupata usingizi wa kutosha ni nguzo muhimu ya maendeleo ya kihisia na kiakili ya mtoto, lakini mara nyingi umuhimu wake hupuuziwa. Ratiba zisizo na mpangilio wa kulala zimehusishwa kwa karibu na changamoto mbalimbali za kitabia, kama vile matatizo ya umakini na utulivu wa kihisia.


Utafiti wa wataalamu mashuhuri wa usingizi wanaobobea katika maendeleo ya watoto unaonyesha kuwa kulala kuna jukumu kubwa katika kuunda afya ya akili na kimwili ya mtoto.


Katika makala hii, tutachunguza athari za kutokulala kwa mpangilio, na kutoa ushauri wa jinsi ya kuweka ratiba bora za kulala kwa watoto.


Dkt. Monique LeBourgeois, mwanasayansi mashuhuri wa usingizi kutoka Chuo Kikuu cha Colorado Boulder, amejikita katika kuchunguza jinsi ratiba zisizo thabiti za kulala zinavyoathiri ubongo wa watoto. Utafiti wake unaonyesha kuwa, kulala bila ratiba thabiti huingilia mzunguko wa kibayolojia wa mwili (circadian rhythms), ambao huathiri utendaji wa kihisia na kiakili kwa watoto.


Matokeo ya Dkt. LeBourgeois yanalingana na maoni ya wataalamu wengine katika uwanja wa utafiti wa usingizi: Kulala mara kwa mara na kwa ratiba thabiti ni muhimu kwa maendeleo ya ubongo wa mtoto. Wakati wa kulala, ubongo unajifunza, huchakata hisia, na huimarisha mifumo ya neva. Kutokulala kwa mpangilio kunavuruga mchakato huu, na kusababisha udhaifu katika umakini, kumbukumbu, na uwezo wa kufanya maamuzi.


Utafiti mwingine wa msingi uliofanywa na Dkt. Yvonne Kelly kutoka Chuo Kikuu cha London uliangazia uhusiano kati ya ratiba zisizo thabiti za kulala na uwezo wa kiakili wa watoto. Utafiti huo, uliowashirikisha zaidi ya watoto 11,000, ulionyesha kuwa watoto waliokuwa na ratiba zisizo thabiti za kulala walipokuwa na umri wa miaka mitatu walikuwa na matokeo ya chini katika masomo ya hesabu, kusoma, na uelewa walipofika umri wa miaka saba. Hii ilithibitisha kwamba athari za ratiba mbaya za usingizi zinaweza kudumu kwa muda mrefu na kuathiri maendeleo ya kielimu.


Ratiba zisizo na mpangilio wa kulala huleta athari za moja kwa moja katika tabia ya mtoto. Kulingana na Dkt. Judith Owens, mkurugenzi wa kitengo cha usingizi katika Hospitali ya Watoto ya Boston, watoto wanaokosa usingizi wa kutosha huwa na tabia kama vile, kushindwa kudhibiti hasira, hali ya kutokutulia (hyperactivity) na kufanya vitu bila kufikiria madhara yake (Impulsiveness). Dkt. Owens anafafanua kuwa kulala vibaya kunaweza kudhoofisha sehemu ya ubongo inayohusika na uwezo wa kufanya maamuzi, umakini, na udhibiti wa hisia (prefrontal cortex).


Matokeo ya kawaida ya kutokua na ratiba thabiti za kulala ni changamoto za umakini. Hata kukosa usingizi kidogo tu kunaweza kupunguza uwezo wa mtoto kusikiliza vizuri shuleni, kuhifadhi mafunzo mapya, na kudhibiti hisia zake. Utafiti unaonyesha kuwa kukosa usingizi kunaweza kusababisha dalili za matatizo ya umakini na utulivu (ADHD), na hivyo kuathiri mafanikio ya watoto kitaaluma na kijamii.


Zaidi ya uwezo wa kiakili, usingizi una jukumu kubwa katika kudhibiti hisia za mtoto. Watoto wanaokosa usingizi huwa na uwezekano mkubwa wa kuwa na mabadiliko ya hisia, tashwishwi, na kushindwa kukabiliana na changamoto za maisha za kila siku.


Aidha, usingizi unasaidia watoto kukuza ujuzi wao wa kijamii. Kukosa usingizi kunaweza kudhoofisha uwezo wao wa kushirikiana na wenzao, na kusababisha migogoro na mtoto kuwa na ugumu wa kuunda urafiki na watoto wenzake. Watoto wanaokosa usingizi pia huwa na wakati mgumu kuonyesha huruma na uvumilivu, sifa ambazo ni muhimu kwa ukuaji katika jamii


Tunawezaje kuwawekea watoto wetu ratiba thabiti za kulala?

Uthibitisho uko wazi, kama tulivyozungumza hapo awali, ratiba zisizo thabiti za usingizi zina athari kubwa kwa maendeleo ya kiakili, kihisia, na kitabia kwa mtoto. Lakini wazazi tunaweza kuhakikisha watoto wetu wanapata usingizi wa kutosha kwa kuweka taratibu sahihi.


Kwanza kabisa kwa kuweka taratibu thabiti za kulala. Kulingana na wataalamu kama Dkt. LeBourgeois na Dkt. Owens, kuwa na ratiba thabiti ya kulala ni moja ya njia bora za kusaidia maendeleo ya kiakili ya mtoto. Jaribu kuweka muda uleule/endelevu wa kulala kila siku, kama ni saa mbili basi iwe saa mbili kila siku hata wakati wa wikendi, ili kusaidia mzunguko wa asili wa usingizi.


Tutengeneze taratibu za kufanya shughuli za  utulivu kabla ya kulala kama vile kusoma vitabu, kusikiliza nyimbo zataratibu, kuoga maji ya moto n.k. Taratibu hizi zinaweza kuashiria ubongo kwamba ni muda wa kulala na mtoto akaweza kulala bila usumbufu. Tujitahidi kuepuka watoto kuangalia runinga au kutumia simu kabla ya kulala  kwasababu zinaweza kuathiri utolewaji wa melatonini, homoni inayodhibiti usingizi.


Tuhakikishe mazingira ya kulala ni mazuri, chumba cha mtoto kinapaswa kuwa kimya, kisafi, chenye giza la kawaida, na katika joto linalofaa. Pia, wakati wa mchana, tujitahidi kuwahamasisha watoto wafanye shughuli za kimwili na mazoezi mepesi, shughuli hizi husaidia watoto kulala kwa utulivu usiku.


Kama tunavyofahamu kuwa watoto hujifunza kwa kuwaangalia watu wazima. Sisi wenyewe tukithamini muda wetu wa kulala hata kama sio muda sawa na mtoto basi kuna uwezekano mkubwa wa watoto kufuata ratiba ya kulala tutakaowapingia.


Tukumbuke kwamba, kulala siyo tu kupumzika; ni mchakato hai unaokuza uwezo wa mtoto kujifunza, kuhifadhi aliyojifunza, kukua, na kufanikiwa katika maisha yake ya baadae hasa katika kudhibiti hisia, kufikiri kabla ya kutenda, kuzingatia masomo na maelekezo ya wazazi, kuhusiana na wenzake, kuwa mtulivu na mwenye umakini katika shughuli zake.


Kwa maoni na ushauri, tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozwi malipo kutoka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook, Instagram na Twitter: @SemaTanzania.

0 views
bottom of page