top of page

Jinsi tunavyoweza kuwasaidia watoto kujitayarisha kwa mitihani na masomo ya kila siku.

  • C-Sema Team
  • Mar 17
  • 3 min read

Kila mzazi anaelewa hisia za wasiwasi na matumaini pale mtoto wake anapokaribia mitihani. Wakati mwingine, tunawaona wakijituma kwa bidii, lakini siku nyingine wanakata tamaa au wanajawa na hofu. Tunajiuliza: Je, tunapaswa kuwasaidia kwa kiwango gani? Au tuwaachie uhuru wa kujifunza wenyewe? Uzuri ni kwamba, msaada wetu unaweza kuwa na mchango mkubwa kwenye mafanikio yao. Leo tutaelezea njia rahisi na zenye ufanisi tunazoweza kutumia kuwasaidia watoto wetu, kujisomea, kujifunza na kujiandaa na mitihani yao kwa utulivu na kujiamini.


Tuhakikishe mazingira yake ya kusomea ni yenye utulivu: Fikiria mazingira ambayo mtoto wako anajaribu kusoma, lakini televisheni inawaka kwa sauti kubwa, simu inatoa miito kila dakika, na vitabu vimechanganyika kila mahali. Je, atasoma kwa umakini katika hali kama hiyo? Ni jambo lililopo ndani ya uwezo wetu kupunguza vishawishi kama simu na televisheni wakati wa kujisomea ili kuwasaidia watoto waweze kuelekeza fikra zao na umakini kwenye masomo

Tuhakikishe miundombinu ya eneo anaosomea ni rafiki: Pawe pasafi na penye mwanga wa kutosha ili mtoto aweze kuzingatia masomo yake. Meza yake iwe safi na ipangwe vyema kwa vitabu, kalamu, daftari, na vifaa vingine muhimu.

Tushiriki kwenye maisha yao ya kujisomea kila siku: Tutenge muda maalum wa kushiriki katika kuwasaidia kufanya kazi za nyumbani walizopewa shuleni. Ukweli ni kwamba, kusubiri hadi siku za mwisho kabla ya mtihani kujiandaa sio mkakati mzuri. Kujifunza ni mchakato unaoendelea, kama vile michezo au mazoezi ya mwili. Tunapowasaidia watoto wetu kuwa na ratiba thabiti ya kujifunza kila siku, tunawajengea nidhamu ya kujiendeleza na kujisimamia wenyewe.

Tusimamie muda wao wanaotumia kujisomea: kutumia vipindi vifupi vya kusoma (dakika 25–45) kisha kupumzika kwa muda mfupi kabla ya kuendelea inaleta ufanisi katika kujibu maswali aliyopewa na kumfanya kufurahia zaoezi la kujisomea bila kufanya mzaha na kuzembe. Tunaweza pia kuwa na kalenda ya masomo ili iwe mwongozo wa kazi zao. Kwa kufanya hivi, tunawasaidia kutokupata msongo wa mawazo wanapokaribia mitihani.


Tuwasaidie kuona kusoma ni jukumu lao muhimu na siyo kazi nzito: tunaweza kufanikisha hili kwa kufanya mambo mbalimbali kama kuwaruhusu wafundishe wenzao; mtoto anayeweza kufundisha mwingine hujiskia fahari na kuongeza bidi katika kujisomea huku ikimhakikishia kuwa ameelewa vizuri. kutumia kadi za maswali na majibu; Hii ni mbinu bora kwa kuhifadhi taarifa muhimu kwa njia ya kuulizana na inampa ari ya kuongeza umakini, kufanya mazoezi ya mitihani iliyopita; hii huwasaidia kuelewa aina na namna ya maswali ambayo huwekwa kwenye mitihani na kujiamini zaidi kukabiliana na mitihani na majaribio, kutumia video au michoro ya maelezo; Watoto wengi hujifunza vyema kwa kuona badala ya kusoma tu maandishi.


Tuwafundishe kusimamia muda wao.Watoto wengi hukabiliwa na changamoto ya kugawanya muda wao kati ya masomo, michezo, na burudani. Tunaweza kuwasaidia kwa kuwafundisha jinsi ya kupanga kazi na kuzifanya kwa awamu ili kuepuka msongo wa mawazo. Kutokana na mambdiliko ya kidijitali, unaweza kufanikisha hili kwa kutumia teknolojia ya Pomodoro, kusoma kwa dakika 25 kisha kupumzika kwa dakika 5. Hii huwasaidia watoto kuwa makini bila kuchoka haraka.


Vipi kuhusu pale mtoto anapokua na hofu ya mtihani?

Hofu ipo, hata sisi watu wazima huwa na hofu hiyo, lakini kusema maneno kama ‘’tulia’’ au ‘’acha uoga’’ kwa mtoto aliye na wasiwasi wa mtihani, mara nyingi haimsaidii. Badala yake, tunaweza kufanya yafuatayo:

  • Kumfundisha mbinu za kupumua kwa kina (breath work). Hii husaidia kupunguza wasiwasi na hofu.

  • Kuhakikisha anapata muda wa kupumzika na. Mwili wenye afya huwezesha akili kufanya kazi vizuri, kwa umakini na utulivu. Hakikisha analala angalau masaa 8 kwa usiku ili akili ipate muda wa kupumzika

  • Kumkumbusha kuwa juhudi yake ndio muhimu na sio matokeo yake pekee. Tunapaswa kusisitiza juhudi badala ya kumfanya aamini kuwa alama ndizo zinamdefine.

  • Kumkumbusha mafanikio yake ya nyuma, Hii inamjenga kuamini uwezo wake.

·        kufanya mazoezi na kula mlo kamili, tunahitaji kuhakikisha watoto wetu wanakuwa katika hali bora kiafya kwa kuhakikisha wanafanya mazoezi na kucheza, wanakula vyakula vyenye virutubisho kama samaki, karanga, mboga za kijani, na matunda na wanakunywa maji ya kutosha ili kuweka mwili na akili katika hali nzuri.

 

Kuhusu teknolojia na mtandao, si kila muda unaotumiwa mtandaoni na watoto hupotea. Kuna zana za kidijitali zinazoweza kuwasaidia kujifunza, kama vile:

  • Khan Academy & BBC Bitesize (kwa ufafanuzi wa masomo tofauti).

  • Quizlet & Anki (kwa kuunda kadi za maswali na majibu).

  • Google Keep & Evernote (kwa kupanga na kuhifadhi noti za masomo).

  • Shule Direct (kwa mitaala ya masomo mbalimbali)


Tuwahimize kutumia teknolojia kwa njia sahihi ili iwe msaada badala ya tatizo kwaokwa kuhakikisha tunawasimamia hasa muda wanaoumia mtandaoni.


Lengo letu kama wazazi si tu kuhakikisha watoto wetu wanasoma, bali pia kuwasaidia kuwa na uwezo na kujiamini katika safari yao ya kujifunza. Kwa kuwapa mazingira bora, kuwasaidia kuunda tabia nzuri za kusoma, na kuwakumbusha kuwa mafanikio ni safari, tunawapa zana zitakazowasaidia maisha yao yote. Tujitahidi kuwa sehemu ya safari yao ya elimu, si wapinzani wao!


Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania; Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org

 

bottom of page