top of page
  • faithmkony

Kizazi chetu bila matatizo ya afya ya akili inawezekana.

Updated: Sep 17


 



Msongo wa mawazo, sonona na changamoto mbalimbali za afya ya akili zimekuwa zikiwatatiza watoto na vijana wadogo kwa wingi hata kuwasababisha kufikia hatua ya kuchukua uhai wao.

Kutokana na kukua kwa kasi kwa janga hili, yatupasa kutathmini namna ya kuepuka changamoto hii na kuvunja muendelezo wake kwa vizazi vyetu endelevu.

 

Wataalamu wa afya ya akili wanaamini kuna mambo ambayo tukiyazingatia kwa watoto wetu katika hatua za ukuaji wao, itawasaidia kuhimili changamoto mbali mbali za maisha ambazo zinaweza kupelekea msongo wa mawazo na magonjwa Kama sonona na unyogovu.

 

Tujitahidi kuwa karibu na kuwafahamu watoto wetu ili tutumie aina ya malezi inayowafaa.

 

Tuwekeze juhudi za makusudi kuwa karibu na watoto wetu ili tuweze kujenga mahusiano thabiti. Hii itakuwa chachu ya kuchochea malezi bora kwa watoto wetu. Mahusiano na watoto wetu yatatusaidia kujua aina sahihi ya malezi ya kuyafuata ili kuwafanya Watoto hawa kuwa watu wa mfano kwenye jamii zetu, na kupalilia mabadiliko chanya hata kwa vizazi vyao.

 

Tunazo aina nyingi za malezi kama vile; malezi ya kimamlaka na uongozi, malezi ya kutelekeza, malezi ya kiutawala na mabavu na malezi ya bora liende. Wataalamu wa afya ya akili wanasema kuwa aina bora ya malezi yatakayomsaidia mtoto  aweze kukua katika misingi imara na ni malezi ya kimamamlaka na uongozi. Hii ni aina ya malezi ambapo mzazi au wazazi wanachanganya udhibiti (kusimamia kanuni na kutoa mwongozo) na huruma, kujali pamoja na ufatiliaji wa mara kwa mara. Mtoto anawekewa mipaka na sheria wazi, huku akionyeshwa  upendo, msaada, kusikilizwa maoni yake na kupewa muongozo kwa ukaribu.

 

Pia watoto wanaadabishwa kwa njia zinazompa nafasi ya kujifunza kutokana na makosa pale ambapo wanakuwa wamekosea. Tujilazimishe kuwapa nafasi ya kujitetea, hii itatusaidia kupata mwanga wa safari yao ya kifikra na mtazamo wao juu ya tukio husika mpaka kufikia hatua iliyopo. Lakini pia tuwape mtazamo wetu ili wapate taswira ya namna wengine tulivyoona na kuchukulia tukio husika ukiachana na mtazamo wao.

 

Mtindo huu wa malezi utawasaidia watoto wetu kukua wakijiamini, kujithamini, kujitambua na, kujikubali. Lakini pia wataweza kujitegemea, kukabiliana na changamoto za maisha na kufanya maamuzi sahihi wakizingatia hisia za watu wengine watakaoguswa kwa namna moja ama nyingine na maamuzi ama matendo yao.

 

Tuwapatie Watoto wetu msaada wa kisaikolojia pale wanapouhitaji.

 

Kila mtoto anahitaji upendo,ushauri na ushirikiano kutoka kwa mzazi wake  ili aweze kukua  vizuri kiafya, kiakili na kihisia. Jambo moja ambalo wazazi wengi hasa katika jamii zetu za Kiafrika hususani Tanzania tunalikosa, ni desturi ya kuwapeleka watoto kwa wataalamu wa saikolojia pale mtoto anapoonesha dalili za magonjwa ya afya ya akili au pale mtoto anapoonesha anahitaji msaada na mwongozo wa maisha.

 

Tufahamu kwamba, mtaalam wa saikolojia anaweza kumsaidia mtoto kugundua kipaji chake,uwezo wake ndani na nje ya shule, pamoja na upekee aliokua nao. Lakini pia humsaidia kujiamini na kufahamu jinsi gani ya kukabiliana na changamoto za kijamii na kiafya kiujumla. Kwa mujibu wa tafiti za kisayansi, watoto na Vijana wanaweza kujieleza zaidi juu ya yale yanayo wasibu kwa mtu ambaye si wa karibu yao hasa mtaalamu wa saikolojia endapo mzazi hakujenga msingi na desturi ya kufanya mazungumzo na mtoto wake tangu akiwa mdogo.

 

Kwa nafasi kubwa zaidi sisi kama wazazi yatupasa tuwe msaada wa kwanza wa kisaikolojia kwa watoto wetu. Kwa mfano; tuweke jitihada katika kutatua matatizo ya kihisia kwa kuwasikiliza mawazo yao, chanzo cha huzuni kwao, na kuwapa ushauri namna ya kuondokana na wasiwasi na woga.

 

Tuhakikishe watoto wetu wanapata lishe bora

Lishe bora ni mlo kamili ambao unajuimisha vyakula vyote vya wanga,protini, mafuta,madini chumvi,vitamini. Fikiria ubongo wa mtoto kama Treni ya mwendokasi (SGR), Ili liendeshwe kwa kasi na ufanisi, inahitaji umeme mwingi na wenye ubora. Hivyo ndivyo lishe bora inavyofanya kwa ubongo wa mtoto ni kama umeme wenye nguvu unaomwezesha kukua, kujifunza, na kufikiri kwa nguvu.

Lishe bora inafanya nini kwa ubongo wa mtoto? Huujenga ubongo vizuri na huchochea shughuli za ubongo ili mtoto afikiri vizuri, ajifunze haraka, na akumbuke vitu kwa urahisi. Tafiti zinaonyesha kwamba ubongo wenye afya nzuri unasaidia binadamu kupigana na magonjwa ya akili kuliko ubongo uliodhoofika kwa kukosa virutubisho (nutrients) muhimu.

 

 

Tuwape Watoto wetu mazingira bora ya kuishi Tuhakikishe mtoto anaishi katika mazingira bora. 

 

Mazingira bora ni kama mfumo wa ulinzi kwa mtoto – yanamlinda mtoto na vile vitu vinavyoweza kumdhuru.

 

Je, mazingira bora yanaweza kumsaidia mtoto vipi kuepuka matatizo ya afya ya akili?

Mazingira ya familia na jamii yenye urafiki na upendo humpa mtoto nafasi ya kujifunza jinsi ya kuhimili  hisia zake kwa njia nzuri na kuamini kwamba watu wa kumsaidia na kumsikikiza wanapatikana katika mazingira yake na hivyo kuwa huru na mwepesi kuomba ushauri na kujieleza kwa wale wanaomzunguka hata akiwa kijana. Mtoto anajifunza jinsi ya kukabiliana na matatizo na mfadhaiko kwa ufanisi.

 

Fikiria mtoto anayekua katika familia yenye upendo na mazingira ya utulivu. Anahisi yupo salama, amezungukwa na watu wanaompenda, na anafursa za kujifunza na kukua. Mtoto huyu ana uwezekano mkubwa wa kuwa na uwezo wa kukabiliana na changamoto za maisha kuliko  mtoto anayekua katika mazingira yenye ukatili na ukosefu wa upendo. Mtoto huyu anauwezekano mkubwa wa kukabiliwa na matatizo ya afya ya akili.

 

Nani mwenye jukumu la kutengeneza mazingira salama? Jibu ni rahisi, sisi wazazi, walezi na jamii kwa ujumla.

 

Tumalize kwa kusema kwamba, kizazi kijacho bila matatizo ya afya ya akili kinawezekana. Lakini, inahitaji juhudi za pamoja, tunahitaji kuwekeza katika malezi bora, mazingira yenye upendo na usalama, na elimu kuhusu afya ya akili tangu watoto wakiwa wadogo.. Tuongeze uelewa wa afya  ya akili, tuondoe ubaguzi, na tuhakikishe kila mtoto anaweza kupata msaada anaohitaji.


Pamoja, tunaweza kujenga kizazi chenye afya ya akili, chenye furaha, na chenye uwezo.

 

Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania; Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org (http://www.sematanzania.org/)

 

 

1 view

Recent Posts

See All

Comments


bottom of page