Lishe duni ni chanzo kikubwa cha magonjwa na vifo vya watoto hapa Tanzania. Kiasi cha watoto 130 hupoteza maisha kila siku kutokana na kukosa lishe bora. Lishe duni hudumaza ukuaji wa watoto kimwili na kiakilli na hivyo kupunguza uwezo wa kufanya vizuri shuleni na pia hupunguza ufanisi katika maisha ya utu uzima.
Yaani madhara ya lishe duni utotoni yanaweza kupelekea matatizo ya kiafya ya kudumu mashani. Tumekuwekea hapa baadhi ya takwimu kuhusu tatizo la lishe na kwa kaisi tumependekeza namna ya kukabiliana na tatizo hili katika ngazi ya familia.
Kiasi cha asilimia 42 (zaidi ya milioni tatu) ya watoto wa Tanzania wa umri wa chini ya miaka mitano wamedumaa kutokana na lishe duni kabla ya kuzaliwa hadi na miaka 2 baada ya kuzaliwa. Udumavu ni wa kiwango cha juu sana katika sehemu nyingi za Tanzania, ikiwa ni pamoja na sehemu mashuhuri kabisa katika uzalishaji wa mazao ya chakula ikiwamo Njombe, Iringa, Kagera na hata Arusha.
Vilevile kiwango cha udumavu Tanzania ni zaidi au karibu sawa na asilimia 40 kwa watu wazima wote isipokuwa tu kwa wenye vipato vya juu wachache wanaokadiriwa kuwa takribani asilimia 20. Ushahidi huu unaashiria kwamba chanzo hasa cha udumavu ni zaidi ya upungufu wa chakula na umaskini wa familia.
Mifano ya madhara ya kiafya kutokana na lishe duni ni pamoja na utapiamlo mkali, ambao kwa Zanzibar pekee asilimia 12 ya watoto wameathirika. Upungufu wa Vitamini A ambao nao ni matokeo ya lishe duni hudhoofisha kinga mwilini na hivyo kuwa chanzo kikubwa cha magonjwa na vifo vya watoto. Anemia (ugonjwa wa upungufuwa damu) kwa kawaida ina uhusiano na malaria pamoja na lishe duni. Anemia isipotibiwa husababisha uchovu na kuathiri uwezo wa kuwa makini na kujifunza. Mwisho ni upungufu wa madini joto, hali ambayo inaathiri ukuaji wa akili, uwezo wa watoto wa kujifunza na kukua vizuri.
Kwa vile lishe duni mara nyingi ni matokeo ya desturi za ulaji (na wala sio matokeo ya upungufu wa chakula) na magonjwa ya uambukizo, tatizo hilo linaweza kutatuliwa kwa kuhimiza uchukuaji wa hatua tano zifuatazo katika kuboresha lishe.
Lishe bora kwa wasichana na wanawake. Wasichana na wanawake wanaopata mlo kamili kabla na wakati wa ujauzito wana uwezekano mkubwa zaidi wa kujifungua watoto wenye afya. Wanawake wanapaswa kupata chakula bora zaidi kilishe wakati wa ujauzito na kutofanya kazi ngumu hasa katika miezi mitatu ya mwisho kabla ya kujifungua. Kuhudhuria kliniki ya uzazi walau mara nne wakati wa ujauzito ni muhimu kwa ajili ya ufuatiliaji wa afya ya mama na ya mtoto ambaye hajazaliwa.
Unyonyeshaji wa mtoto mchanga maziwa ya mama pekee kwa miezi sita ya mwanzo. Maziwa ya mama humpatia mtoto viinilishe, vitamini na madini yote muhimu kwa ukuaji wake katika kipindi cha miezi sita ya mwanzo, na mtoto hahitaji kinywaji wala chakula cha aina nyingine yoyote. Nchini Tanzania ni nusu tu ya vichanga ndio inayonyonyeshwa maziwa ya mama pekee kwa miezi 2 hadi 3, na kiwango hicho kinashuka hadi asilimia 23 tu kwa watoto wa umri wa miezi 4 hadi 5.
Kwa upande wa Tanzania bara wastani wa umri wa vichanga vinavyonyonyeshwa maziwa ya mama pekee ni miezi 2.4 ili hali kwa Zanzibar ni wiki mbili tu. Watoto wachanga wa umri wa chini ya miezi 6 wanapopewa maji au vyakula vingine huwa katika hatari ya kupata maambukizo huku wakikosa kingamwili inayopatikana katika maziwa ya mama kwa ajili ya kuwakinga na magonjwa.
Baada ya mtoto kutimiza miezi 6 apewe vyakula vya kulikiza vyenye lishe bora. Mara nyingi watoto hupatwa na tatizo la utapiamlo wanapokuwa na umri wa kati ya miezi 6 na 23 kutokana na kutopata mara kwa mara aina mbalimbali za vyakula vyenye lishe bora.
Vyakula wanavyopewa zaidi watoto mara nyingi huwa ni vya aina ya wanga na watoto huwa hawapati mbogamboga, matunda na protini ya kutosha. Watoto wadogo pia wanahitaji kula mara kwa mara (mara nyingi kwa siku) kuliko watu wazima. Milo midogomidogo ya mara kwa mara na yenye lishe bora ni mizuri zaidi kwa mtoto kuliko mlo mmoja au miwili mikubwa.
Urutubishaji wa vyakula. Kula chumvi yenye madini joto pamoja na vyakula vingine vilivyoongezwa virutubisho kama vile unga wa ngano, unga wa mahindi na mafuta ya kupikia yaliyoongezwa vitamini na madini kutaboresha lishe ya wanafamilia wote na hasa watoto. Juhudi kubwa zinaendelea za kutengeneza unga laini maalumu wenye virutubisho ambao utauzwa kwa familia kwa bei nafuu na ambao utafaa kuongezwa moja kwa moja kwenye vyakula vya watoto ili kuongeza viinilishe muhimuu kwa ukuaji wa miili ya watoto.
Hatua dhidi ya ugonjwa wa kuharisha na malaria. Magonjwa yote haya mawili ni chanzo kikubwa cha utapiamlo. Kuboresha usafi wa mazingira ya nyumbani, hasa kwa kuhakikisha kwamba kila mwanafamilia ananawa mikono kwa sabuni kila anapotoka chooni, kabla ya kuandaa na kula chakula na baada ya kumsafisha mtoto kutapunguza kwa kiasi kikubwa ugonjwa wa kuharisha. Kila familia haina budi kuwana choo kinachotunzwa vizuri pamoja na upatikanaji mzuri wa maji salama. Watoto na mama wote wajawazito wanapaswa kulala kwenye vyandarua vyenye dawa, homa zitibiwe haraka bila kucheleweshwa na mama wajawazito watumie vidonge vya kujikinga na malaria.
Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org.