top of page
C-Sema Team

Kwa nini ulinzi wa watoto ni muhimu zaidi katika msimu wa likizo?

Tunapoendelea kufurahia kipindi hiki cha likizo pamoja na watoto wetu, ni muhimu kuelewa kuwa msimu huu wa sherehe pia huleta changamoto zinazoweza kuhatarisha usalama na ustawi wa watoto. Furaha ya msimu wa sikukuu inaweza kugeuka kuwa changamoto ikiwa hatua za uangalizi wa watoto hazitachukuliwa kwa umakini.


Katika kipindi hiki, watoto hutumia muda mwingi wakicheza, kusafiri, au kushiriki katika matembezi na familia. Ingawa haya ni mambo mazuri, yanaweza pia kuwa chanzo cha hatari kama vile ajali, kupotea kwa watoto, au hata ukatili na unyanyasaji. Kwa sababu hiyo, ni jukumu la wazazi, walezi, na jamii kwa ujumla kuimarisha ulinzi wa watoto ili kuhakikisha wanasherehekea kwa furaha, salama na amani .

Changamoto zinazoweza kuwakumba watoto wakati wa sikukuu na likizo.

Ajali za barabarani: Msimu wa sikukuu huongeza msongamano wa magari na watu, na mara nyingi watoto huathirika kutokana na ajali ambazo zingeweza kuepukika kwa uangalizi wa karibu.


Kupotea kwa watoto: Watoto huweza kupotea wanapokuwa kwenye maeneo yenye mikusanyiko mikubwa kama masoko, viwanja vya michezo, au sehemu za burudani. Lakini pia wahalifu hutumia fursa hii kutekeleza njama zao ovu za kuteka na kupoteza watoto.


Unyanyasaji wa watoto: Kuna ongezeko la matukio ya unyanyasaji wa watoto, iwe kimwili, kihisia, au kingono, wakati wa sikukuu. Hali hii inaweza kuzuilika kwa uhamasishaji wa jamii na ulinzi wa karibu wa watoto hasa kuanzia ngazi ya familia.


Usalama wa mitandao: Watoto wengi hutumia muda mrefu kwenye simu au vifaa vya kielektroniki, na hii huongeza hatari ya unyanyasaji wa kimtandao au kufikiwa na kuwasiliana na watu wenye nia mbaya.


Ili kuhakikisha watoto wanasherehekea sikukuu kwa furaha na usalama, ni vyema tukafuata hatua zifuatazo:


Kwanza tuwaelimishe kuhusu usalama kwa kuwaeleza mbinu na hatua rahisi za usalama, kama vile kutoondoka nyumbani bila ruhusa, kutozungumza na watu wasiowajua, kutotembea nje ya nyumbani usiku bila usimamizi wa mtu mzima na kuepuka maeneo hatarishi kama vile vichaka, mapori, maeneo yenye ujenzi na kuwa makini wanapokuwa kwenye mikusanyiko n.k


Pili, tuwe na uangalizi wa karibu na watoto wetu ndani na nje ya nyumba. Tuhakikisha kwamba watoto wanapokuwa katika maeneo ya burudani kama fukwe za bahari, viwanja vya michezo, au hata nyumbani, wako chini ya uangalizi wa mtu mzima mwenye jukumu la kuhakikisha usalama wao.


Usalama wa mitandao pia ni jambo ambalo tunapaswa kulitazama, katika zama hizi za teknolojia, wazazi wengi hupenda kupakia picha na video za watoto kwenye mitandao ya kijamii. Ingawa ni njia nzuri ya kujiburudisha na kuhabarisha tuwe makini na maudhui tunayochapisha, kwani yanaweza kutumiwa vibaya na watu wenye nia mbaya.


Pia, tuangalie matumizi ya watoto ya simu na vifaa vingine vya kielektroniki ili kuhakikisha wanatumia teknolojia  na mitandao ya kijamii kwa usalama bila kuhatarisha faragha yao. Katika kukabiliana na hili hakikisha unazima GPS (mfumo wa kusoma mahali mtu au kitu kilipo) za simu na tablet na vifaa vingine vya kielektroniki ili kuzuia wahalifu kutambua mahali alipo mtoto wakao kwa wakati fulani na epuka kuweka taarifa binafsi za familia na za mtoto pia. Inashauriwa kupost matukio yaliyopita, kwa mfano picha za mtoto au familia ikiwa fukweni leo zinapostiwa kesho yake au wakisharudi nyumbani ili kuwanyima wahalifu fursa ya kufuatilia nyendo za familia.


Miwsho tuhakikishe watoto wanafahamu namba za dharura mfano namba ya hudua ya simu kwa mtoto (116), namba ya polisi (112) na namba ya jeshi la zima moto (114), pamoja na maeneo wanapoweza kupata msaada ikiwa kuna changamoto au tatizo lolote.


Tukumbuke kwamba usalama wa watoto si jukumu la mzazi pekee bali la jamii kwa ujumla. Tunaposherehekea, tuchukue muda kuhakikisha watoto wetu wanabaki salama. Furaha ya mtoto inapaswa kuwa ya kudumu, na hatupaswi kuruhusu msimu wa sikukuu kugeuka kuwa chanzo cha majuto, kwani kinga ni bora kuliko tiba!


Kwa maoni na ushauri kuhusu masuala ya watoto, piga simu namba 116 bila malipo. Pia, unaweza kututembelea kupitia mitandao yetu ya kijamii: Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania, au tovuti: www.sematanzania.org.


2 views
bottom of page