Disemba ni mwezi ambao umejaa sikukuu nyingi na pia ni mwezi ambao watoto hufunga shule na kurejea nyumbani kwa ajili ya mapumziko ili kusherehekea sikukuu hizi pamoja na familia zao. Makala haya yanaangazia namna ambavyo mzazi anaweza kumlinda mtoto wake dhidi ya mambo mbalimbali yanayoweza kuathiri ustawi wa mtoto katika kipindi hiki.
Kwakuwa watoto hutumia muda mwingi shuleni, kipindi cha likizo ni fursa adhimu kwa wazazi na walezi kutenga muda wa kutosha kukaa na watoto kubadilishana mawazo. Hii itakusaidia kufahamu mabadiliko chanya na hasi yaliyojengeka kipindi ambacho hukuwa na fursa ya kumfuatilia mwanao na kumpatia muongozo bora pamoja na kumsifia pale utakapoona anafanya mambo yenye tija kulingana na alichojifunza shule.
Ikumbukwe kuwa watoto wakiwa shule kuna vitu wanavikosa kama vile kucheza kwa muda mrefu na marafiki zao, kutembeleana, kuangalia vipindi vya luninga na filamu, kuwatembelea ndugu na jamaa, kuhudhuria sherehe mbalimbali n.k. Ni vyema kabisa na ni haki yao ya msingi kupata uhuru wa kuyatimiza yote haya lakini yanahitaji muongozo kutoka kwa wazazi na walezi.
Ni muhimu wazazi kutoa mwongozo wa namna watoto watakavyotumia muda wao wakati wa likizo bila kuathiri haki zao za msingi kwa mujibu wa sheria. Wape watoto uhuru wa kufurahia filamu na vipindi vya luninga huku ukihakikisha vipindi hivi vina maadili kulingana na umri. Hakikisha unawafahamu fika marafiki wanaotembeleana na kucheza nao; mtoto anafanya nini akiwa nje ya nyumba? Fahamiana na wazazi wa marafiki wa wanao na hakikisha familia za ndugu anaokwenda kuwatembelea zinazingatia malezi yenye maadili na si kujikuta mtoto anashinda kwenye vibanda vya video akiangalia picha zisizo na maadili au kulala kwenye sherehe zisizo na maadili na kujihusisha na michezo na marafiki wasiofaa kwa makuzi bora ya mtoto.
Zingatia usalama wa watoto katika kipindi hiki ambacho ajali nyingi pamoja na vitendo vya ukatili kwa watoto hutokea ikiwemo utoroshwaji, usafirshwaji haramu na upotevu wa watoto. Uangalizi utahitajika zaidi hasa pale watoto wanapokuwa katika mazingira ya sehemu za burudani za watoto. Zingatia sana muda wa kucheza na kurejea nyumbani.
Shirikiana na mwanao kutengeneza ratiba nzuri kwa siku zote za likizo yenye uwiano kati ya mambo ya burudani na shughuli za kujifunza. Burudani inaweza jumuisha ratiba ya kuangalia vipindi vya luninga, kutembelea sehemu maalum za michezo ya watoto, kuzuru mbuga za wanyama, na michezo mbalimbali kama vile mpira n.k. Ratiba ya shuguli za kujifunza inaweza jumuisha mazoezi ya maswali ya masomo kulingana na darasa analosoma, kutembelea maktaba kwaajili ya kujisomea vitabu, kuwafundisha watoto stadi za kazi na maisha amabzo zinaendana na umri wao na zinazozingatia mazingira halisi ya maeneo wanapoishi. Mfano, kupika, kuwahudumia wanyama wa kufugwa nyumbani na mengineyo.
Wazazi hawapaswi kuwaruhusu watoto wao kufanya kila kitu wanachotaka badala yake, wawashauri ni kipi bora katika hivyo wanavyovitaka. Ni muhimu sana kwa mzazi kujua mambo mtoto anayofanya kwa kuwa hii itamsaidia kutambua iwapo anajihusisha na mambo ambayo ni hatarishi kwa afya na makuzi yake. Ni muhimu pia kwa watoto kushauriwa kuepuka vishawishi hasi kutoka kwa marafiki na makundi rika. Hii inaweza kusaidia mtoto kujilinda na hatari ya kufanyiwa ukatili.
Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org