top of page
  • C-Sema Team

#SimuliziZa116: Jirani asaidia mtoto kurudi kwa wazazi wake Dodoma

Tarehe 2 Agosti 2018 tulipokea simu kutoka Ilala Dar es salaam ambapo jirani aliyeonesha kukerwa alitusimulia kisa cha mtoto Anitha (sio jina halisi) mwenye umri wa miaka 9. Binti huyu anatokea Mkoa wa Dodoma na alichukuliwa kutoka kwao Dodoma kwa ahadi ya kuja kusomeshwa jijini Dar es salaam.



Baada ya kuwasili jijini Dar es salaam ahadi ilibadilika na badala yake aligeuka na kuwa mfanyakazi wa nyumbani kwa mama huyo. Tulielezwa kuwa binti Anitha alifungiwa ndani kuanzia asubuhi mama huyo alipoondoka kwenda kazini mpaka jioni aliporejea jambo ambalo lilimsukuma huyu jirani yake kutafuta msaada ili kumuokoa binti huyu mdogo kwani mazingira aliyokua akiishi hayakua rafiki kabisa hasa kwa umri wake kuwa mdogo.


Tuliwasiliana na ofisi ya Ustawi wa Jamii Ilala na alipatikana afisa aliyepanga kwenda mtaani alikoishi Anitha ili kuthibitisha madai ya mtoa taarifa wetu. Baada ya kuona ni kisa cha kweli, Afisa Ustawi wa Jamii aliwasiliana na wazazi wake waishio Mkoani Dodoma na kuwaita Dar es salaam kwa ajili ya kumchukua binti yao.


Tarehe 10 Agosti 2018 Afisa Ustawi wa Jamii aliwasiliana nasi na kutueleza kuwa binti Anitha amerejeshwa katika mikono salama ya wazazi wake na tayari yuko Dodoma.


Sheria ya Mtoto inatamka wazi kuwa ni wajibu wa kila mwanajamii ambaye ana ushahidi au taarifa kwamba haki za mtoto zinakiukwa au mzazi, mlezi na ndugu anayemlea mtoto ana uwezo, lakini hataki kumpatia mtoto chakula, malazi, haki ya kucheza na kufurahi, mavazi, huduma za afya na elimu au kumtelekeza, kuripoti suala hilo kwenye mamlaka ya Serikali za Mitaa ya eneo hilo. Usikae kimya! Tupigie simu namba 116 tuzungumze!

0 views

Comentários


bottom of page