top of page
  • C-Sema Team

#SimuliziZa116: Mtoto Aisha apata matibabu!

1/3/2018 tulipokea simu toka Sengerema, Mwanza iliyopigwa na baba mzazi wa mtoto kutaka msaada kwani mwanae, Aisha (jina lake halisi tumelihifadhi) alisumbuliwa na tatizo la kichwa kikubwa (Hydrocephalus). Aisha alikuwa na umri wa mwaka mmoja wakati alipopelekwa hospitali ya Bugando kwa ajili ya matibabu. Baba Aisha alisema alitakiwa kutoa pesa shilingi 150,000/- ambazo hakuweza kuzipata.



Alipojaribu kuchangisha kwa ndugu na rafiki zake wengi walimshauri kuwa anapoteza muda kwani mwanae huyo karogwa hatibiki hospitali. Hivyo Baba Aisha alimpeleka mwanae kwa 'mtaalamu' wa kuagua, yaani mganga wa kienyeji ila bado hali ya mtoto haikutengamaa.

HiVyo aliamua atupigie Huduma kwa Mtoto. Tulimpigia Bi. Janet Manoni toka Friends of Children with Cancer ambaye husaidia watoto wenye matatizo ya kiafya kama vile saratani na vichwa vikubwa. Bahati nzuri alikuwa yuko Mwanza wakati huo na alimtafuta Baba Aisha na mara moja alimsaidia kupata huduma ya vipimo hospitalini Bugando.

Mtoto alifanyiwa vipimo na waliambiwa hakuna haja ya upasuaji anatakiwa kufanya mazoezi kama sehemu ya tiba, vilevile wakampa na kiti maalumu cha kukalia kwa ajili ya mazoezi. Walishauriwa kurudi hospitalini hapo baada ya miezi miwili kuangalia maendeleo ya mtoto.

Baba alipiga simu kutushukuru baada ya kupata huduma hizo kwa mtoto wake!


Tunatoa shukurani zetu za dhati kwa Bi Janet Manoni na timu yake Friends of Children with Cancer kwa kuwa pamoja nasi kila tunapowatafuta kutoa msaada kwa watoto kama Aisha. Pamoja tunaweza! Tupigie simu namba 116 tuzungumze! ^ @SemaTanzania

0 views

Comments


bottom of page