top of page
  • C-Sema Team

#SimuliziZa116: Mtoto mfanyakazi za nyumbani aliyegeuzwa mke


Mama mmoja alitupigia simu namba 116 kutoa taarifa juu ya binti yake aliyekuwa amesafirishwa kutoka Songea kuja Dar es Salaam kufanya kazi kama #Mfanyakazi za nyumbani. 'Nina wasiwasi sana juu ya maisha ya mwanangu, siwezi hata kulala vizuri siku hizi tangu siku niliyoambiwa kwamba sasa hafanyi tena kazi za nyumbani bali amegeuzwa mke wa mtu huko mjini.' 'Tafadhali nisaidieni.' Aliongeza mama huyu.

Makubaliano ya kumsafirisha mtoto yalifanyika kati ya mumewe ambaye ni baba-wa-kambo wa binti yao na 'mwajiri' ambaye alimwahidi baba-mtu fedha nzuri tu ikiwa atakubali kuruhusu mtoto kwenda kuishi naye mjini kama #Mfanyakazi. Mwanaume huyo mwajiri pia aliahidi kumpeleka binti shule akiwa mjini ili 'kumuendeleza'.

Mama wa mtoto alidai hakuhusishwa kabisa katika mipango hii. Alipijaribu kuuliza alihadaiwa na mumewe kuwa rafikiye wa mjini amejitolea kumsomesha binti yao mjini. Hata hivyo, baadaye mama aligundua kuwa huu ulikuwa uongo na kwamba bintiye mwenye umri wa miaka 17 amegeuzwa mke huko mjini wala haendi shule.

Tuliazimia kufanya uchunguzi kwa kushurikiana na vyombo vya dola ili kubaini ukweli wa taarifa hizi. Binti alipatikana Temeke Dar es salaam na kweli aliishi na mwanaume huyo 'mwajiri / mume'. Dawati la Jinsia na Watoto Polisi Temeke walimfikisha binti hospitali kwa uchunguzi wa kitabibu na kuthibitisha kuwa aliingiliwa kingono na bahati nzuri hakuwa na maambukizi ya magonjwa ya zinaa (STDs). Vilevile uchunguzi ulibaini kuwa hakuwa na ujauzito.

Mtuhumiwa (mwajiri / mume) alifunguliwa kesi ya kubaka na usafirishaji haramu wa mtoto huku baba wa mtoto akifunguliwa kesi ya kushiriki katika usafirishwaji haramu wa mtoto wake.

Sasa mama wa mtoto tayari amekutanishwa na binti yake na wote ni mashahidi muhimu katika kesi hii.

Tupigie namba 116 bila malipo maalumu kutoa taarifa za namna hii zinazoweza kuwasaidia mabinti na hata watoto wengine wanaopitia madhila mbalimbali mijini na vijijini kote Tanzania bara na visiwani. Simu yako inaweza kuokoa maisha ya mtoto. ^ @SemaTanzania

0 views

Comments


bottom of page