top of page
C-Sema Team

Umuhimu wa baba kumsindikiza mama kliniki


Umuhimu wa baba kumsindikiza mama kliniki

Ingawa akina baba walio wengi sasa wanajua umuhimu wa kuwasindikiza wazazi wenza (akina-mama) kliniki wakati wa ujauzito na hata baada ya kujifungua, bado wapo wengi wenye dhana kuwa kupima afya zao ndiyo lengo pekee la kwenda kliniki.


Wengi walio na dhana hii pia huwategemea akina mama kupima afya wenyewe na baada ya matokeo mazuri hujiaminisha kuwa wao ni salama pia. Hii dhana ni potofu kwani yanayofanyika kliniki za uzazi ni zaidi ya upimaji wa afya. Yapo mambo mazuri muhimu ambayo akina baba wakiyajua ni faida sana kwao, lakini hasa kwa watoto wao. Hivyo ni muhimu sana kwa mama kuhudhuria kliniki mara tu anapogundua kuwa ni mjamzito. Makala haya yamekuchambulia baadhi ya manufaa ya baba kumsindikiza mama kliniki.


Mosi ni kujua afya ya mama na baba ili kumlinda mtoto mtarajiwa. Wakati wa kiliniki wajawazito na wenza wao hushauriwa kupitia vipimo mbalimbali kujua hali za afya zao ambapo itasaidia pia kumlinda mtoto mtarajiwa ikiwa itagundulika mmoja ya wazazi au wote wanaugua magonjwa mbalimbali ikiwemo kuishi na virusi vya UKIMWI.


Kwenda pamoja kliniki humfanya mama kuwa na furaha na kufurahia ujauzito alionao. Kwamba mwenzi wake anamjali na kumthamini na hivyo kuona thamani ya kiumbe alichokibeba. Tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa mama hujisikia furaha mno akigundua kuwa mume wake anampenda na kumjali hasa kipindi cha ujauzito.


Husaidia baba kuongeza uelewa wa majukumu yaliyoko mbele yake ikiwemo lishe bora kwa mama ili mtoto tumboni akue vizuri. Kliniki za uzazi pamoja na mambo mengine hutolewa ushauri wa lishe bora kwa mama hivyo baba anapokwenda na mama kliniki atapata kujua ni aina ya vyakula adhimu kwa mama wakati na baada ya kujifungua. Hii humsaidia kumkumbusha na kumsisitiza iwapo atajisahau.


Humsaidia baba kuelewa mabadiliko ya kimaumbile na mara nyingine tabia kwa mama. Akijua vyema atapata fursa nzuri kuishi naye kwa upendo na uvumilivu hasa katika kipindi cha ujauzito. Wakati wa ujauzito mama anaweza kubadilika kitabia akawa na hasira au kumchukia yeyote bila sababu. Baba atapata fursa ya kusikia uzoefu wa akina baba wenzake awapo kliniki na kujipanga kuishi na kutoa huduma kwa mwenza wake. Huna haja ya kukimbia nyumbani wakati wa ujauzito wa mama kwa kuogopa malumbano. Jifunze toka kliniki.


Hujenga mahusiano mazuri kati ya baba na mtoto atakaezaliwa. Tafiti zinaonyesha kwamba mtoto hushiriki furaha aliyonayo mama. Mama mwenye furaha, mtoto mwenye furaha. Haiwezekani usimpende akiwa tumboni eti unasubiri azaliwe ndio uanze mahusiano naye. Siku njema huonekana asubuhi. Mtoto awapo tumboni anapata hisia zake toka kwa mama yake. Uwepo wako karibu na mama mjamzito, ni sawasawa na kuwa karibu na kijacho wenu. Umbali wako na kijacho wenu utahitaji nguvu ya ziada ya kujenga mahusiano pindi akizaliwa. Anza mapema!


Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116 ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania; Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org

8 views
bottom of page