Malengo ya elimu kwa mtoto yanategemea sana ushirikiano baina ya waalimu na wazazi. Katika suala zima la elimu ya mtoto, wazazi na waalimu tunapaswa kushirikiana ili kufikia lengo kuu, ambalo ni kuona watoto wanajifunza kwa ufanisi na kufanya vizuri katika masomo yao na katika maisha yao ya baadae.
Licha ya kuwa na lengo hili bado kuna changamoto za hapa na pale katika kujenga ushirikiano kati ya wazazi na waalimu. Utafiti unaonesha kuwa mawasiliano na ushirikiano imara kati ya wazazi na walimu huathiri moja kwa moja utendaji wa mtoto kitaaluma na kitabia.
Mazingira ya nyumbani na shuleni ndiyo yanayoongoza maisha ya mtoto kwa nafasi kubwa. Mazingira haya mawili yanapofanya kazi pamoja, mtoto anapata faida nyingi kwa njia tofauti: Kwanza kabisa mafanikio ya kitaaluma. Utafiti wa National Education Association (NEA) unaonesha kuwa wanafunzi ambao wazazi wao wanahusishwa kikamilifu katika elimu yao huwa na alama za juu, mahudhurio bora, na huwa na stadi bora za kijamii.
Pili, watoto huwa na mabadiliko chanya ya tabia. Utafiti wa mwaka 2016 uliochapishwa kwenye The School Community Journal uligundua kuwa watoto ambao wazazi wao walijenga na kudumisha mawasiliano mazuri na thabiti na walimu wao walikuwa na uwezekano mdogo wa kuwa na matatizo ya kitabia.
Jambo la tatu ni ukuaji wa kihisia na kijamii. Mahusiano ya ushirikiano kati ya wazazi na walimu huwasaidia watoto kujenga hisia za usalama, wakijua kuwa wale watu wazima muhimu katika maisha yao wamejipanga kuwasaidia katika ukuaji wao pale watakapopitia changamoto zozote shuleni na nyumbani.
Je, wazazi tunawezaje kushirikiana vyema na walimu ili kutengeneza mazingira yatakayowawezesha watoto wetu kujifunza vizuri?
Kujenga ushirikiano mzuri kati ya wazazi na walimu si jambo linaloweza kufanyika mara moja—huhitaji jitihada, mawasiliano ya wazi, na kuheshimiana. Wazazi tunaweza kufuata mbinu zifuatazo;
Tuanzishe mawasiliano ya wazi mapema, tusisubiri mikutano ya wazazi na walimu au changamoto za kitaaluma kutokea. Tuanze kujenga uhusiano na walimu wa watoto wetu mwanzoni mwa mwaka wa masomo pale tu tunapokwenda kuwaandikisha/kuwasajili shuleni. Kisha tuwe tunafuatilia na kujadliana mara kwa mara maendeleo ya mtoto na changamoto zozote pamoja na mafanikio yote ya mtoto. Pia tujitahidi kuonesha nia ya kutaka kuwasaidia watoto wetu katika safari yao ya elimu.
Tushiriki moja kwa moja katika masuala ya mtoto shuleni, mfano, kuhudhuria hafla za shule, kujitolea kwa hali au mali inapowezekana, na kuonyesha nia ya dhati ya kutaka kufahamu maisha ya kitaaluma ya watoto wetu. Hii haitatusaidia tu kuwa na taarifa za watoto lakini pia inawaonesha watoto wetu kuwa elimu ni kipaumbele.
Tujitahidi kuheshimu mchango na mawazo ya walimu. Penda tusipende walimu wanautaalamu wa kipekee wa kutoa muongozo au ushauri kama jinsi sisi wazazi tuna utaalamu wetu wa malezi. Sisi tunawafahamu watoto wetu vizuri lakini walimu pia wanaleta maarifa ya kitaalamu juu ya mikakati ya kielimu na mienendo ya watoto darasani. Tukiwachukulia walimu kama wasaidizi badala ya wapinzani, tutaimarisha ushirikiano wetu.
Ikiwa changamoto imetokea tuwakabili walimu kwa mtazamo wa kushirikiana badala ya kugombana nao.
Kulingana na aina ya changamoto, tunaweza kutoa maoni yetu kwa heshima na kuuliza mtazamo wao pia. Kwa pamoja, tunaweza kubuni mikakati ya kushughulikia changamoto hizo kwa ufanisi.
Tunaelewa kuwa kuna muda ratiba na shuguli zetu zinatubana na kufanya mawasiliano ya mara kwa mara kuwa magumu. Ila tunaweza kujitahidi kutumia simu au barua pepe kuzungumza au kutuma jumbe fupi kurahisisha mawasiliano kati yetu na walimu wa watoto wetu.
Na kuna wakati mwingine wazazi huwa tunakuwa na wasiwasi kuhusu kuzungumza na walimu, tukihofia kuhukumiwa au kutokuwa na uhakika wa jinsi ya kutimiza mahitaji ya kielimu ya watoto wetu. Lakini inatubidi kujenga ujasiri na kuwa na mazungumzo ya wazi na walimu na hata uongozi wa shule kuhusu changamoto hizo.
Ili watoto wetu waweze kufanya vizuri katika safari yao ya elimu, hatuna budi bali kushirikiana na kujenga mahusiano mema na walimu wao.
Kwa maoni na ushauri, tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozwi malipo kutoka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook, Twitter na Instagram @SemaTanzania.