Stories

Hizi hapa dalili za awali za ujauzito

Last updated one year ago

Hizi hapa dalili za awali za ujauzito

Je, bado una wasiwasi kuwa yawezekana ukawa mjamzito? Kwa kweli njia pekee kujua kama wewe ni mjamzito ni kupima ujauzito.

Hata hivyo, zipo dalili za awali zinazoweza kukujulisha kuwa yawezekana ukawa mjauzito.

Je, wajawazito wote huwa wanapata dalili za kufanana?

Ukweli ni kwamba wanawake hawapati dalili za kufanana, kila mwanamke yuko tofauti. Vivyo hivyo ndivyo zilivyo dalili zake za ujauzito. Pia ikumbukwe kwamba hata kwa mwanamke huyo huyo aliyewahi kuwa mjamzito, dalili za kila ujauzito zinaweza zisifanane.

Tahadhari nyingine muhimu ni kuwa inawezekana kabisa dalili za awali za ujauzito zikashabihiana na dalili za kuingia na ukiwa kwenye hedhi, hivyo unaweza usitambue kwa urahisi kwamba umepata ujauzito.

Endelea kukaa nasi sasa ili tukupitishe hatua moja kwenda nyingine katika kupitia dalili hizi za awali za ujauzito ambazo kama huu sio ujauzito wako wa kwanza haya ni marudio. Kumbuka dalili hizi pia zinaweza kusababishwa na sababu zingine ambazo hazitokani na ujauzito. Hivyo kule kuona tu dalili hizi haimaanishi kwamba wewe ni mjamzito, njia pekee ya wewe kujua ni kupitia kipimo cha ujauzito.

Maumivu ya tumbo la uzazi pamoja na kutokwa na matone ya damu ukeni.

Baada ya upevushaji wa yai, yai lililorutubishwa hujipandikiza kwenye mji wa mimba. Hii inaweza kusababisha dalili za awali za ujauzito ambazo ni kama kutokwa na matone ya damu na wakati mwingine maumivu ya tumbo la chini ya kitovu.

Matone hutokana na kujipandikiza kwa yai lililorutubishwa kwenye mji wa mimba. Hutokea wakati wowote ndani ya ya siku 12 baada ya yai kurutubishwa.

Maumivu ya tumbo la uzazi (chini ya kitovu), huwa yanashabihiana na maumivu ya hedhi, hivyo baadhi ya wanawake huyachukulia kama maumivu ya hedhi.

Pamoja na kutokwa damu ukeni unaweza kuona ute mweupe mwepesi kama maziwa kutoka ukeni. Ute huu huwa hauna madhara wa harufu na hauambatani na kuwasha. Pale unapokuwa na  wasiwasi kuhusu ute huu unaweza kumwona daktarin naye atakufanyia vipimo kuona kama una fangasi, bakteria au kalamidia.

Ute huu unatoka wapi? Baada ya kutungwa mimba, seli za kwenye kuta za uke huongezeka uongezeka unene. Kuongezeka huku kwa seli za kwenye kuta za uke ndiko kunakosababisha ute huu wa kutoka ukeni.

Ute huu huwa unaendelelea katika kipindi chote cha ujauzito.

Mabadiliko katika matiti.

Mababdiliko katika matiti ni dalili nyingine ya awali ya ujauzito. Kiwango chako cha vichocheo (hormone) huwa kinapanda kwa kasi baada ya upevushaji. Mabadiliko hayo yanaweza kufanya matiti kujaa, kuwa kama na vitu vinavyochoma choma au hata kuwa na vidonda wiki moja au mbili baada ya urutubishwaji. Unaweza kuhisi uzito kwenye matiti au matiti kuuma yanaposhikwa. Sehemu nyeusi ya chuchu huwa nyeusi zaidi.

Kuna sababu zingine zinazoweza kusababisha mabadiliko katika matiti. Ikiwa mabadiliko haya yanatokana na ujauzito basi kuwa na hakika kwamba itachukuwa muda kwa vichocheo kuzoeleka na vitakapozoeleka maumivu nayo huwa yanapungua.

Uchovu.

Uchovu wa kupindukia katika kipindi cha ujauzito ni jambo la kawaida na ambalo huwa linaanza mapema tu katika wiki za awali za ujauzito.

Unaweza kujihisi mchovu  mara tu baada ya kutungiwa mimba.

Kwa nini unachoka? Hii hutokana na kiwango kikubwa cha kichocheo cha progesterone. Ifahamike kuwa uchovu pia unaweza kusababishwa na sababu zingine kama vile kushuka kwa shinikizo la damu, kushuka kwa kiwango cha sukari kwenye damu au pia ongezeko kwenye uzalishaji wa damu.

Kama uchovu wa kupindukia unatokana na ujauzito ni vema upange kupata mapumziko ya kutosha. Ulaji wa vyakula vyenye ukwasi mwingi wa protini na madini ya chuma unaweza kusaidia kuondoa au kupunguza tatizo hili.

Kichefuchefu.

Hii ni dalilil maarufu na iliyozoeleka ya ujauzito. Hata hivyo si kweli kwamba kila mjamzito hupata kichefuchefu.

Sababu halisi ya kichefuchefu haijulikani ingawaje kupanda kwa vichocheo katika kipindi hiki cha ujauzito kunaweza kuwa moja ya sababu. Kichefuchefu katika kipindi cha ujauzito kinweza kutokea wakati wowote ule ila mara nyingi hutokea wakati wa asubuhi.

Mbona wajawazito huchagua chagua sana chakula? Kweli kabisa baadhi ya wajawazito hupenda baadhi ya vyakula na huchukia vingine. Hii pia ni kwa sababu ya mabadiliko ya vichocheo mwilini. Hali hii ya kichefuchefu inaweza kuwa kubwa kiasi kwamba hata vyakula pendwa navyo havikai tumboni. Hali hii inaweza kuwa mbaya kwa baadhi ya wanawake kiasi cha kuhitjai huduma ya matibu ya kulazwa hospitalini.

Mara nyingi kichefuchefu, kutamani baadhi ya vyakula au kuchukia baadhi ya vyakula kunaanza kupungua kuanzia wiki 13 ya ujauzito kwa wajawazito wengi. Hali hii kwa baadhi ya wajawazito inaweza kuendelea katika kipindi chote cha ujauzito.

Katika kipindi hiki kumbuka kula lishe yenye uwiano mzuri ili wewe na mwanao muweze kupata virutubisho vinavyotakiwa. Unaweza kuwasiliana na daktari kwa ushauri zaidi kuhusu chakula unachohitajika kula.

Kukosa kuona siku (hedhi).

Kutokuona hedhi nayo ni dalili ya awali iliyozoeleka ya ujauzito.  Tafiti zinaonesha kuwa hii moja ya sababu kuu ya kwafanya wengi kukimbilia kupima ili kujua kama kweli ni wajwazito. Hata hivyo, fahamu kwamba kutokuona siku (hedhi) au hedhi kuchelelwa siyo lazima itokane na kuwa una ujauzito.

Kumbuka uwapo mjamzito unaweza kutokwa na damu ukeni hivyo ni vizuri ukamuuliza daktari wako kama kutokwa damu kupi ni dalili ya hatari na kupi ni kwa kawaida.

Jua kwamba zipo sababu zingine tofauti na ujauzito zinazoweza kuchangia wewe kutokuona hedhi. Baadhi ya sababu hizi ni kuwa na ongezeko kubwa la uzito wa mwili, mabadiliko ya vichocheo (hormone), uchovu kupindukia, msongo, n.k. Baadhi ya wanawake huwa wanakosa hedhi zao baada ya kusitisha matumizi ya dawa za uzazi wa mpango. Kama umechelewa kuona siku na unahisi ni mjamzito pima ujauzito kuwa na hakika.

Dalili zingine za awali za ujauzito

Ujauzito huambatana na mabadiliko katika kiwango cha uwiano wa vichocheo katika mwili wa mama. Tofauti ya uwiano huu huweza pia kusababisha dalili zingine mfano: -

  • Kukojoa mara kwa mara ambako kwa wanawake wengi huanza wiki ya sita au ya nane baada ya kutungwa mimba. Hata hivyo ni vizuri kukumbuka kuwa kukojoa mara kwa mara kunaweza kusababishwa na maambukizi katika njia ya mkojo (UTI), kunaweza kusababishwa na ugonjwa wa kisukari na mara kadhaa kunaweza kusababishwa na matumizi ya dawa za diuretiki zinazotumika kushusha shinikizo la juu la damu.

 

  • Kukosa choo. Katika kipindi cha ujauzito kiwango cha juu cha progesteroni kinawaweza kusababisha kukosa choo. Hii ni kwa sababu progesteroni husababisha chakula kupita taratibu tumboni. Unashauriwa kunya kunywa kiasi kikubwa cha maji, kula vyakula vyenye utajiri mwingi wa ufumwele (foods rich in fiber).

 

  • Mababdiriko katika uchangamfu (moody swings). Hali hii ni kawaida katika miezi mitatu ya kwanza. Hali hii pia inachangiwa na mabadiliko ya vichocheo.

 

  • Maumivu ya kichwa na mgongo. Uwapo mjamzito unaweza kupatwa na maumivu kiasi ya kichwa na pengine unaweza kupata maumivu ya mgongo.

 

  • Kizunguzungu na kuzirai. Vyote viwili vinaweza kuwa vimechangiwa na kutanuka kwa mishipa ya damu kunakopelekea kushuka kwa shinikizo la damu. Hali hii pia inaweza kusabaishwa na kushuka kwa kiwango cha sukari kwenye damu.

Mwisho. Uwapo mjamzito unaweza usiwe na dalili hata moja ya zilizotajwa hapo juu. Vilevile unaweza ukawa na dalili zote hizo kwa pamoja. Pale ambapo dalili mojawapo au zote zinakuletea maudhi basi wasiliana na daktari kwa ufumbuzi.

Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116 ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania, Instagram @sematanzania na www.sematanzania.org

Picha na Pregnancy.Org