Last updated 10 months ago
Akina mama wengi huwa wana wasiwasi kama wana maziwa ya kutosha. Katika siku za kwanza baada ya kujifungua mama huwa anatoa maziwa ya njano ambayo huwaitwa dang'a au kolostramu (colostrum). Maziwa haya ni muafaka kwa mtoto kwani huwa yana antibodi zinazosaidia kumlinda mtoto wako mchanga dhidi ya maradhi. Lakini pia husaidia kuandaa tumbo kwa ajili ya umeng'enyaji wa maziwa.
Watoto wengi huwa wanapoteza kiwango kidogo cha uzito katika siku 3 mpaka 5 za mwanzo baada ya kuzaliwa. Hata hivyo kupungua huko kwa uzito hakutokani na unyonyeshaji hivyo huna haja ya kuhamaki.
Maziwa huwa yanaongeza kadri hitaji la chakula (maziwa) linapoongezeka. Watalaamu wa afya hupendekeza maziwa ya mama pekee mpaka umri wa miezi 6. Endelea kumpa maziwa hata kama hayatoki nae puka kumchanganyia maziwa ya kopo kwani hupunguza utokaji wa maziwa.
Hata pale ambapo maziwa yako ni machache au unadhani hayatoshi ni vyema ukaendelea kumnyonyesha mwanao. Unaweza ukaamua kumnyonyesha mwanao kwa wakati fulani tu kuliko kuacha kabisa. Hata hivyo wasiliana na daktarin atakuelezea njia za kuongeza maziwa kwani wakati mwingine siyo suala la maziwa machache bali ni jinsi unavyomuweka mtoto wako kwenye titi.
Njia za kumpakata na kumuweka mtoto vizuri kwenye titi apate wingi wa maziwa.
Kumuweka mtoto katika njia inayotakiwa humsaidia mama na mtoto kukaa katika mkao wa kustarehe. Kukaa huku kutasaidia maziwa ya mama kutoka vizuri na mtoto atapata maziwa ya kutosha. Fuata ushauri huu: -
Nifanyeje kuhakikisha mtoto amekavaa vizuri kwenye titi?
Kukaa vizuri kwenye titi kutamwezesha mwanao kupata maziwa ya kutosha na ili hili litokee ni lazima akae mkao utakaomwezesha kupokea ziwa vizuri bila ya kugeuza shingo yake wakati wa kunyonya. Tumia mkono mmoja kushika titi lako kisha gusisha chuchu yako kwenye mdomo wa chini wa mwanao. Namna hiyo mtoto atafunua mdomo wake wazi. Atakapokuwa amepanua kwa kiwango cha mwisho sukumiza ziwa lako katika mdomo wake uliyo wazi juu ya ulimi.
Utajua kuwa mwanao amekaa vizuri kwenye ziwa pale ambapo mdomo wote utakuwa umebinukia nje na sehemu nyeusi ya chuchu iliyo kubwa itakuwa upande wa juu. Wakati mtoto akinyonya mama anaweza kuthibitisha kama mwanae amekaa vizuri kwa kuangalia vifuatavyo.
Ila kama mtoto hajakaa vizuri kwenye ziwa atanyonya muda mrefu na akiachia atalirudia na ukimtoa kwenye ziwa atalia. Hivyo mtoe na umuweke tena vizuri kwenye ziwa. Kumbuka kutomuweka mtoto vizuri huchangia mama kupata vidonda kwenye chuchu. Namna hii mtoto hukosa lishe ya kutosha na huwa hashibi.
Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116 ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania, Instagram @sematanzania na www.sematanzania.org
Picha ni kwa hisani ya gazeti la Habari Leo.