Stories

Wazazi tukumbuke haki za mfanyakazi wa nyumbani

Last updated 4 years ago

Wazazi tukumbuke haki za mfanyakazi wa nyumbani
Wafanyakazi wa nyumbani ni wasaidizi au watekelezaji wa kazi zote za nyumbani kwa kuzingatia uhusiano wake na aliyemwajiri. Usaidizi wa kazi za ndani ni moja kati ya kazi za zamani sana na kimsingi inalenga sana jinsia ya kike ingawa kwa kiasi fulani hata wanaume pia huajiriwa kufanya kazi hizi. Hata hivyo ni moja ya sekta isiyo na usimamizi wala maendeleo kwa kuwa katika nchi nyingi sheria za kazi hazitumiki kuwalinda wafanyakazi wa nyumbani.   Ni wazi kwamba wazazi (waajiri) ni mashahidi wakubwa juu ya kazi lukuki wanazofanya wasaidizi hawa wa nyumbani kila siku ikiwa ni pamoja na kufanya usafi wa nyumba na mazingira yake, kupika, kufua, kulea watoto pamoja na ulinzi wa nyumba. Tatizo ni kwamba kwa kiwango kikubwa wafanyakazi hawa hukumbwa na changamoto nyingi katika kutekeleza majukumu yao ikiwemo kupigwa, kunyimwa chakula, kufanyishwa kazi nyingi kuliko uwezo wao na hata kubakwa na kuingilia kinyume na maumbile.   Wengi wetu husahau mchango mkubwa wa wafanyakazi wa nyumbani katika familia na jamii zetu kwa ujumla. Ajira zao ni za manyanyaso na wamekua wakiongezeka na kuhitajika kila kukicha ingawa maslahi yao yanazidi kuwa duni. Wimbi la changangamoto zinazowakabili limeendelea kushika hatamu licha ya kwamba sheria za kazi zinawatambua. Makala haya yanalenga kuwaelimisha wazazi kuweza kutambua haki za wafanyakazi wa nyumbani ili kujenga dhamira madhubuti ya kutekeleza haki hizi kwa vitendo.   Kwa kuzingatia sheria ya Ajira na mahusiano kazini namba 6 ya mwaka 2004, ambapo wafanyakazi wa nyumbani wamejumuishwa pamoja na wafanyakazi wengine, haki wanazostahili kupewa ni hizi zifuatazo:-   Haki ya kupewa likizo. Ni muhimu kutambua kuwa wafanyakazi wa nyumbani ni binadamu, na kama binadamu wengine, huwa wanachoka hivyo kupata likizo ni haki ya msingi kwao. Tulijaribu kufanya utafiti mdogo na kugundua kua, wafanyakazi wengi wa nyumbani hufanya kazi kila siku pasipo kupumzika, hali hii huwafanya wengi wao kusingizia kuwa ni wagonjwa ili wapate muda wa kupumzika. Ni idadi ndogo sana ya wazazi ambao huwapatia wasaidizi wao wa ndani likizo. Ifike wakati wazazi tujenge nia ya dhati katika kutoa likizo kwa wasaidizi wetu wa ndani ili kuheshimu utu wao.   Kuchangiwa katika mifuko ya hifadhi ya jamii ni haki wanayostahili kupewa wafanyakazi wa nyumbani. Wasaidizi wa kazi za ndani ni watunzaji wakubwa wa familia hasa kwa wazazi ambao ni watumishi wa umma au binafsi wakati wanapoondoka nyumbani. Kama wewe ulivyo na haki ya kuchangiwa katika mfuko wa hifadhi na mwajiri wako, ni muhimu kuwaandikisha wafanyakazi wetu wa ndani kwenye mifuko ya jamii. Hii ni haki yao kwa kuwa wasaidizi hawa ni sawa na wafanyakazi wengine na wanastahili kupata mafao yanayotokana na mifuko hiyo.   Kupewa mikataba ya kazi ni haki stahiki ya wafanyakazi wa nyumbani. Kwa muda mrefu sasa wasaidizi wa nyumbani wamekua wakifanya kazi bila kuwa na makubaliano maalumu ya mikataba. Matokeo yake ni kwamba hukumbwa na dhahama ya kuachishwa kazi kila kukicha kwa kuwa hawana chochote kinachowalinda. Ipo haja ya kuwapa mikataba ili kujenga uhakika katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku wawapo kazini.   Wafanyakazi wa nyumbani wanayo haki ya kulipwa mishahara yao kamili na kwa wakati. Ni jambo la kusikitisha kuona wazazi wakiwacheleweshea au kutowalipa ujira wasaidizi wa nyumbani, hii siyo sahihi bali ni kuwanyima haki zao za msingi. Uzoefu unaonyesha kuwa wazazi wengi hutoa hoja za kwamba wamekua wakiwahifadhi wafanyakazi hao katika nyumba zao hivyo hawaoni haja ya kuwalipa mishahara. Huu ni uonevu na ukandamizaji wa juu unaopaswa kupingwa vikali.   Yatupasa kutambua kuwa wafanyakazi wa nyumbani ndiyo walinzi na hubeba uhai wa familia zetu. Wanao uwezo wa kuiangamiza au kuistawisha familia. Tuthamini mchango wao kwa vitendo na nia ya dhati tofauti na hali ilivyo sasa.   Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania; Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org